Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amewataka madiwani wa vyama vya upinzani kujiunga na CCM ili waweze kushirikiana naye kutekeleza ilani ya uchaguzi ya chama tawala.
Amesema yupo tayari kupokea simu ya diwani wa CCM hata akipigiwa usiku wa manane, ili kumpa msaada lakini si diwani kutoka vyama vya upinzani.
Akizungumza jana Februari 11, 2018 katika mkutano wa hadhara kata ya Haydom wilayani Mbulu, Mnyeti amesema ni vyema madiwani wa Chadema wakajiunga na CCM.
Amesema diwani wa Chadema ni ngumu kufanikisha maendeleo ya wananchi kwa madai kuwa, hakuna ambaye atamsikiliza akiwasilisha hoja zake katika vikao vya halmashauri husika.
"Hata hapa Haydom najua ni ngome ya Chadema hata mwenyekiti wa kijiji namuona ana damu ya CCM, sasa ondokeni huko mje huku tutekeleze ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 hadi 2020 kwa kuleta maendeleo," amesema Mnyeti.
Awali, mkazi wa kata ya Hayderer, John Tluway aliuliza swali kwa mkuu huyo wa mkoa akitaka kujua sababu za mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga kutofika kwenye kata hiyo inayoongozwa na Chadema.
Akijibu swali hilo, Mnyeti amempongeza Mofuga kwa kutokufika kwenye kata hiyo inayoongozwa na Chadema kwa maelezo kuwa diwani wa kata hiyo anapaswa kujiunga na CCM ili kufanikisha maendeleo.
"Mkuu wa wilaya ninakupongeza kwa wewe kutofika kwenye kata hiyo kwani ningepata taarifa umefika mara ya kwanza, mara ya pili na mara ya tatu ningekuwa na mashaka na wewe lakini hongera sana kwa kutokwenda," amesema Mnyeti.
Pia, amewataka watumishi wa halmashauri hiyo kutekeleza na kufanikisha kwa vitendo ilani ya CCM hata kama hawana kadi ya chama hicho kwani ndicho ambacho kipo madarakani.
"Mtekeleze hayo kwa nia safi, hiyo ni sawa na imani kwani hata kanisani huwezi kusikia padri akimsifu Muhammad na pia kule msikitini imamu huwa hamsifu Yesu," amesema Mnyeti.
Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Mbulu, Nasaeli Sulle alimhakikishia Mnyeti kuwa wananchi wa Haydom wamejitambua kuwa walifanya makosa na kuchagua Chadema ila sasa wapo tayari kuwachagua viongozi wanaotokana na CCM.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment