KAMPUNI ya Grumeti Fund kupitia idara yake ya maendeleo ya jamii Leo mei 28,2023 imeadhimisha siku ya hedhi salama duniani kwa kutoa msaada wa taulo za kike zenye thamani ya zaidi ya million 8, zinazoweza kutumika kwa kipindi Cha mwaka mmoja na nusu (reusable pads) kwa zaidi ya wanafunzi wa kike 640 kutoka katika shule za sekondari Serengeti na Nyichoka zilizopo wilayani Serengeti mkoa wa Mara.
Akikabidhi msaada huo mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii ya kampuni ya Grumeti Fund, Frida Mollel amewasihi wasichana hao kuwa hedhi sio ugonjwa bali ni kitu cha asili kwa mwanamke na hakipaswi kuwa sababu ya kuzuia binti kufikia ndoto zake.
"Grumeti Fund imeona sababu ya kuwapatia mabinti taulo za kike leo ili waweze kujisitiri na kujitunza na kuzingatia masomo yao ili kutimiza ndoto zao"amesema Frida.
kwa upande wa mkufunzi kutoka chuo cha afya Kisare Mwl.Restuda Murutta amewasisitiza wanafunzi hao kuzingatia usafi wawapo katika kipindi cha hedhi ili kuepuka madhara yanayoweza kutokana na uchafu wakati wa hedhi na utupaji sahihi wa taulo za kike.
"tusitupe taulo zetu katika vyoo vya maji hii inasababisha kuziba kwa choo pia ni vizuri kuzingatia usafi hasa kuosha via vya uzazi na tusitumie sabuni zenye kemikali kwani ni hatari kwa afya ya uzazi "
Aidha wanafunzi hao wameelimishwa juu ya kukabiliana na mimba za utotoni kwa kuchukua tahadhari kwa kuondokana na tamaa za kumiliki vitu pamoja na kutokuwa na makundi mabaya.
kwa upande wao wanafunzi wakieleza sababu zinazoweza kupelekea mimba za utotoni wamesema kukosa elimu ya kijinsia pamoja na kukosa hofu ya Mungu ni baadhi ya visababishi vikubwa vya mimba za utotoni.
"wasichana wengi tunakosa elimu ya kijinsia kwani kutokana na mabadiliko wasichana tunawahi kupevuka hivyo katika kipindi hiki tunakosa elimu ya kijinsia. Pia wanafunzi hao wamesema kuwa "kukosa hofu ya Mungu ni tatizo kwani ukijua hili unalofanya ni kosa mbele za Mungu hutaweza kufanya mambo yatakayosabisha mimba za utotoni".alisema Gladys michael
Naye Mgeni rasmi katika mafunzo hayo Bi.Antusa Swai ameipongeza taasisi ya Grumeti Fund kwa kuadhimisha siku ya hedhi salama duniani kwa kutoa taulo za kike na mafunzo kwa wasichana hao.
"naipongeza sana taasisi ya Grumeti Fund kwa kutoa taulo hizi za kike,zitawasaidia kwa kipindi chote na msijiingize katika vitendo vibaya na kuwa tamaa kwa kukosa mahitaji muhimu cha msingi ni kuwa wavumilivu na kutumia rasilimali zilizopo ili ziwasaidie na hatimaye kuweza kutimia ndoto zenu" alisema Antussa
Grumeti Fund itaendelea kutoa elimu ya kijinsia kwa wavulana na wasichana wa shule za sekondari na kutoa taulo za kike kwa kila binti atakayeshiriki mafunzo hayo. Grumeti Fund inatarajia kuwafikia zaidi ya wavulana na wasichana 3,800 kwa mwaka huu 2023.
No comments:
Post a Comment