Jukwaa la wahariri nchini Tanzania limeazimia kutoandika ama kutangaza habari zozote zinazomuhusisha mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya kiongozi huyo kudaiwa kuvamia kituo cha habari cha Clouds akiwa ameambatana na askari wenye silaha ili kutoa amri ya kurushwa hewani kwa kipindi cha televisheni.Marufuku hiyo ambayo pia inaungwa mkono na umoja wa klabu za waandishi wa habari Tanzania, itaendelea mpaka pale itakapotangazwa ama kuamriwa vinginevyo, wakuu wa jukwaa hilo wamesema.
Katibu wa jukwaa la wahariri nchini Tanzania Nevile Meena, amesema jukwaa hilo limekerwa na hatua ya afisa huyo wa serikali kuamuru kurushwa hewani kwa kipindi cha televisheni sambamba na kutumia nguvu kupora kipindi mali ya Clouds TV.
Kando na kutangaza kwamba halitatangaza au kuandika habari zozote zinazomuhusu Makonda, jukwaa hilo pia limemtaja kama adui wa uhuru wa vyombo vya habari.
Mkanda wa video za siri yaani CCTV wa usiku wa Machi 17, 2017 katika studio za Clouds unaonesha mtu anayedaiwa kuwa Bw Makonda akiingia katika ofisi za kampuni ya Utangazaji ya Clouds iliyopo Dar es salaam, akiwa ameambatana na askari polisi pamoja na maafisa wenye silaha.
Mpaka sasa hajazungumza lolote kuhusu suala hilo.
Rais John Magufuli alisema katika hotuba yake Jumatatu alipokuwa akizindua ujenzi wa barabara ya juu eneo la Ubungo, jijini Dar es Salaam kuwa Bw Makonda aendelee kuchapa kazi na kwamba yeye hafanyii kazi maneno ya kwenye mitandao kwa sababu yeye ndiye rais wa nchi.
Dkt Magufuli alisema kuwa kuna baadhi ya watu wanaingilia majukumu yake wakati yeye ndiye mwenye uamuzi na kwamba hapangiwi kazi ya kufanya kwa sababu anajiamini.
No comments:
Post a Comment