WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wazidi kuiombea Serikali kwani kazi ya kutumbua majipu ina mitihani mikubwa. “Tulikuwa hatufikii lengo kutokana na kuwa na wafanyakazi serikalini ambao walikuwa wanatorosha mali za serikali, lakini hao ndio tunakufa nao,” alisema Majaliwa na kuongeza kuwa serikali imekuwa ikifuata sheria na utaratibu pasipo kumuonea yeyote wakati wa utumbuaji majipu hayo.
Waziri Mkuu alisema hayo jana mjini hapa wakati akiwa mgeni rasmi kwenye sherehe za kumsimika Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelist Assemblies Of God Tanzania (EAGT), Dk Abel Mwakipesile. Askofu Mwakipesile anakuwa Askofu Mkuu wa Kanisa hilo baada wa Askofu wa kwanza Moses Kulola kufariki Agosti 29, 2013.
Pia Waziri Mkuu alizungumzia suala la kuboresha elimu ya msingi na sekondari na kubainisha kuwa kuanzia Julai serikali itaongeza fedha kwa ajili ya mpango wa elimu bure. Majaliwa alisema ni muhimu kuiombea Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imekuwa ikisimamia uwajibikaji kwani utumbuaji majipu unahitaji maombi zaidi kutokana na kuwa na mitihani mingi.
“Wengi hawapendi kuguswa maslahi yao, mtuombee kazi ya kutumbua majipu ni ngumu,” alisema na kuongeza kuwa serikali itafanya kazi kwa kufuata sheria na taratibu na haitamuonea mtu.
Alisema ni takribani siku 100 sasa tangu Rais John Magufuli awe madarakani, lakini amefanya mambo mengi na anatakiwa kuungwa zaidi mkono. “Serikali inaanza kupitia maeneo yote muhimu yatakayofanya Watanzania kupata huduma kwa ukamilifu na moja ya maeneo yatakayoangaliwa katika bajeti ijayo ni kupunguzwa kwa vifaa vya gharama ya ujenzi,” alisema.
Pia alisema zipo baadhi ya taasisi za dini zinazotumia vibaya nafasi za kuingiza bidhaa bila ushuru na kuwanyima fursa wale wenye malengo mazuri. “Tunafuatilia taasisi zinazotumia mgongo wa dini kupitisha vitu visivyo halali,” alieleza.
Aidha, alisema atakuwa na kikao na viongozi wa dini zote maaskofu, mashehe na wachungaji ili kujadili mambo gani yanayotakiwa kufanywa kati yao na serikali ili kuwa kitu kimoja. Aliwaasa watumishi wa serikali kufuata kanuni na sheria katika kuhudumia wananchi wenye matatizo mbalimbali.
“Mwananchi apokelewe, asikilizwe na ahudumiwe na kama huduma haipo kwake aelekezwe kwa kuipata, na kama kuna mtumishi anaona hawezi hayo atupishe, kwani tunataka kuona Watanzania wanapata huduma iliyo bora,” alibainisha Waziri Mkuu.
Alisema kama kuna mtumishi ambaye anaona haendani na kasi ya utendaji kazi ya Serikali ya Awamu ya Tano apishe kwani kuna wasomi wengi wanaohitaji ajira. Pia alisema kuendelea kutoa huduma nzuri lazima mapato ya serikali yanayokusanywa yasimamiwe na kukusanywa kwa ufasaha.
Waziri Mkuu alisema anajua kuna kundi litakasirika kutokana na utendaji kazi wao, na kuongeza, “wanaosema hii ni nguvu ya soda wanajidanganya, hii sio nguvu ya soda. Najua kuna kundi litakasirika kwani tumedhamiria na jitihada zetu ni kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa zinarudi kwa ajili ya kusaidia wananchi.
“Bajeti ijayo ya serikali fedha nyingi zaidi zitapelekwa kwenye maboresho ya elimu nchini na kuanzia Julai tutaingiza kwenye bajeti ili suala hilo liwe endelevu,” alisema akizungumzia mpango wa elimu bure.
Aliwataka Watanzania kuwa wavumilivu kwani mkakati wa serikali katika kuboresha elimu ni mzuri, lakini umeanza na changamoto nyingi, lakini wataendelea kuboresha kutokana na serikali kuwa na mpango mzuri kwenye jambo hilo. Pia alisema ubora wa elimu utaendelea kuimarishwa.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelist Assemblies Of God Tanzania (EAGT), Dk Mwakipesile alisema kanisa hilo lina malengo ya aina mbili ambayo ni ya kiroho na kimwili. Alisema kwa sasa kanisa hilo lina jumla ya makanisa 5,000 Tanzania nzima huku wakiwa na majimbo zaidi ya 90 na Kanda tisa.
Alisema pia kanisa hilo lina miradi mbalimbali ya kijamii pamoja na kiuchumi. ‘’Watanzania wana matumaini na serikali katika kuboresha huduma za jamii hivyo harakati za kutumbua majipu zinawapa matumaini kuwa fedha zitaenda kuboresha huduma za jamii,” alisema Askofu Mkuu Dk Mwakipesile.
Naye Katibu wa EAGT, Leonard Mwizarubi alisema kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ inaleta hamasa kubwa kwa kanisa, kwani wanaamini uchumi utaimarika. “Endeleeni kuchukua hatua mbalimbali za kuleta unafuu wa maisha tupo nyuma yako Hapa ni Kazi Tu,’’ alieleza.
No comments:
Post a Comment